Thursday, November 1, 2012
NASAHA ZA KUHIFADHI QURAN SEHEMU YA PILI
04 Nasaha Za Kujitayarisha Kuhifadhi Qur-aan
Kabla ya kuanza kuhifadhi Qur-aan jitayarishe kwa kwanza kwa kutekeleza wasia ufutao:
Kutia niya yenye ikhlaasw
Anza na kutia niya ya dhati kwamba unataka kuhifadhi Qur-aan kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kutegemea fadhila na malipo yake, na hivi ndivyo inavyopasa katika ibada na vitendo vyetu vyote.
Azimio Na Imani Yakini
Weka azimio thabiti, usichoke, usikate tamaa wala usivunjike moyo utakapoona kwamba unazorota katika baadhi ya Aayah au Surah utakazoziona ngumu. Weka azimio kama mfano unataka kupanda mlima na kufikia kilele chake, ikiwa itakuchukua miezi au hata miaka almuhimu uazimie kufikia tu.
Endeleza hifdhw kwa azimio thabiti japokuwa utakwenda mwendo wa kobe na kumbuka kuwa kitendo chema kinachoendelezwa ni kipenzi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) japo ni kidogo mno:
قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( أحب الأعمال إلى الله أدومها وإن قل)) متفق عليه
Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Vitendo Anavyovipenda Allaah zaidi (kuliko vyote) ni vile vinavyodumishwa japokuwa ni vidogo)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kuomba du'aa
Kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwezeshe kuhifadhi maneno yake. Muombe katika nyakati za kukubaliwa du'aa kila siku, kila mara, Yeye Ndiye mpokeaji du'aa zetu na Ndiye Mwenye kututaqabalia.
Kubakia katika Taqwa (Ucha Mungu)
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
((وَاتَّقُوا اللَّهَ وَيُعَلِّمُكُمُ اللَّهُ))
((Na mcheni Allaah Anakuelimisheni)) [Al-Baqarah: 282]
Kwa hiyo jisafishe kwanza na madhambi kwa kuomba maghfirah kwa Mola Mtukufu, kisha jiepushe na maasi yote kwani maasi yanamzuia mja kushika maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema:
" إن الرجل ليحرم العلم بالذنب يصيبه "،
"Hakika mtu hunyimwa elimu kwa dhambi anazozitenda"
Imaam Ash-Shaafi'iy (Rahimahu-Llaah) alikuwa mwepesi wa kuhifadhi Qur-aan lakini Qur-aan ilipokuwa nzito kuihifadhi alisema:
"شكوت الى وكيع سوء حفظي فأرشدني إلى ترك المعاصي و أخبرني بأن النور علم و نور الله لا يؤتاه عاصي"
"Nililalamika kwa Wakiy’i kuhusu kushindwa kuhifadhi Qur-aan akaninasihi kuacha maasi na akanijulisha kuwa mwanga ni elimu na mwanga wa Allaah haumfikii mwenye kuasi"
Kutoshughulika na anasa za dunia
Inampasa mwenye kutaka kuhifadhi Qur-aan auhifadhi wakati wake mwingi kwa ajili ya kuhifahdi Qur-aan. Ajitenge na anasa za dunia asizichanganye na kazi hii, ili akili yake, na moyo wake upate utulivu kwa ajili ya hifdhwul-Qur-aan. Ni muda mwingi leo hii watu hupoteza masaa mengi kutazama televisheni na kukaa mabarazani au kwenye nyumba zilizotawaliwa na mazungumzo ya kidunia yasiyokwisha.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((مَا جَعَلَ اللَّهُ لِرَجُلٍ مِّن قَلْبَيْنِ فِي جَوْفِهِ))
((Allaah Hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake)) [Al-Ahzaab: 4]
Kipaumbele kwa wakati maalumu kila siku
Ni lazima ujiwekee wakati maalumu kila siku iwe ni kipaumbele katika ratiba zako za kila siku kwa ajili ya kuhifadhi Qur-aan. Na wakati bora kabisa ulioonekana kuwa ni muwafaqa kwa hifdhw ni nyakati za ukimya ambazo hakuna vishawishi vya kukukatiza hifdhw yako, kama simu, watu ingia toka, sauti nyinginezo zozote, na nyakati nzuri ni zile za usiku, karibu na alfajiri, au alfajiri kabla ya kujaza lolote jengine katika bongo lako.
Subscribe to:
Posts (Atom)

