Powered By Blogger

Tuesday, October 30, 2012

NJIA ZA KUKUWEZESHA KUHIFADHI QURAN. (01)

01 Fadhila Za Kuhifadhi Qur-aan. Hifdhwul-Qur-aan (kuhifadhi Qur-aan) hakika ni jambo muhimu la kuazimiwa na Muislamu kwani fadhila zake ni nyingi na tukufu mno. Makala katika kiungo kifuatacho inaelezea fadhila hizo kwa kirefu: 02 Qur-aan Ni Uongofu Kamili Qur-aan ni Kitabu Alichotuteremshia Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kutoka mbinguni, nacho kwetu ni; nuru (mwanga) unaotunawirisha, kamba nene, nzito isiyokatika, mizani ya uadilifu, poza ya moyo, uongofu kamili, na sababu ya furaha na kufaulu kwa binaadamu katika dunia yake na akhera yake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala): ((الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلاَوَتِهِ أُوْلَئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ) ((Wale tuliowapa Kitabu, wakakisoma kama ipasavyo kusomwa, hao ndio kweli wanakiamini)) [Al-Baqarah: 121] 03 Umri Bora Wa Kuhifadhi Qur-aan Umri mzuri utakaorahisisha kuhifadhi Qur-aan ni baina ya umri wa miaka mitano hadi ishirini na tatu taqriban, kwani binaadamu katika umri huu huweza kuhifadhi kwa wepesi kabisa na bongo huwa na kumbukumbu nzuri bado na sio wepesi kusahau unachokihifadhi. Amesadikisha maneno yake ambaye amesema: "الحفظ في الصغر كالنقش في الحجر، والحفظ في الكبر كالنقش على الماء " "Kuhifadhi udogoni ni kama nakshi katika jiwe, na kuhifadhi ukubwani ni kama nakshi katika maji. Maana yake ni kuchora au kuandika katika udongo uliomaji bado, maandishi au mchoro huo hubakia milele kuwa ni alama katika jiwe litakapokauka. Ama mwenye kuchora katika maji, hutoweka. Hivyo ni fursa tukufu Muislamu kuitumia katika umri huu kuhifadhi maneno ya Mola wake, na kama fursa hii imekupita basi wahifadhishe watoto wako wa kiume na wa kike usiache fursa hii ikawapita na wao pia kwani furaha ya wao kuhifadhi Qur-aan itakuwa ni furaha na fakhari kwako pamoja na ridhaa ya nafsi yako. Vile vile mzazi mwenye kumhifadhisha mwanawe Qur-aan atakuwa ameshatanguliza huko Akhera akiba na fadhila zake na za mwanawe. Hata hivyo, endapo utakupita umri huo kusiwe ni sababu ya kukufanya usiweze kuhifadhi Qur-aan, kwani hii ni sababu wengi wanaitumia kwamba akili ni dhaifu ya kuhifadhi au umri ushakuwa mkubwa akili haikamati n.k. Hakika hakuna sababu yoyote ya kumzuia mtu asiweze kuhifadhi Qur-aan, kwani haya ni maneno ya Mola wetu Mtukufu Aliyetuumba na Ambaye Ametuahidi kwamba ni maneno mepesi kuhifadhi kwa yule mwenye dhamira khaswa. Allaah Amerudia ahadi Yake mara nne katika Surah moja: ((وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ)) ((Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur-aan iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anayekumbuka?)) [Al-Qamar: Aayah Namba 17, 22, 32 na 40] Kwa hiyo inampasa mtu awe na imani, yakini na maneno ya Mola Wetu, kuwa na dhana njema, kuwa na matumaini na matarajio mazuri daima, na hivi ndivyo itakavyokupa nguvu zaidi ya kuhifadhi hadi ufikie upeo wake. SOMO LITAENDELEA........