Thursday, November 1, 2012
NASAHA ZA KUHIFADHI QURAN SEHEMU YA PILI
04 Nasaha Za Kujitayarisha Kuhifadhi Qur-aan
Kabla ya kuanza kuhifadhi Qur-aan jitayarishe kwa kwanza kwa kutekeleza wasia ufutao:
Kutia niya yenye ikhlaasw
Anza na kutia niya ya dhati kwamba unataka kuhifadhi Qur-aan kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kutegemea fadhila na malipo yake, na hivi ndivyo inavyopasa katika ibada na vitendo vyetu vyote.
Azimio Na Imani Yakini
Weka azimio thabiti, usichoke, usikate tamaa wala usivunjike moyo utakapoona kwamba unazorota katika baadhi ya Aayah au Surah utakazoziona ngumu. Weka azimio kama mfano unataka kupanda mlima na kufikia kilele chake, ikiwa itakuchukua miezi au hata miaka almuhimu uazimie kufikia tu.
Endeleza hifdhw kwa azimio thabiti japokuwa utakwenda mwendo wa kobe na kumbuka kuwa kitendo chema kinachoendelezwa ni kipenzi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) japo ni kidogo mno:
قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( أحب الأعمال إلى الله أدومها وإن قل)) متفق عليه
Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Vitendo Anavyovipenda Allaah zaidi (kuliko vyote) ni vile vinavyodumishwa japokuwa ni vidogo)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kuomba du'aa
Kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwezeshe kuhifadhi maneno yake. Muombe katika nyakati za kukubaliwa du'aa kila siku, kila mara, Yeye Ndiye mpokeaji du'aa zetu na Ndiye Mwenye kututaqabalia.
Kubakia katika Taqwa (Ucha Mungu)
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
((وَاتَّقُوا اللَّهَ وَيُعَلِّمُكُمُ اللَّهُ))
((Na mcheni Allaah Anakuelimisheni)) [Al-Baqarah: 282]
Kwa hiyo jisafishe kwanza na madhambi kwa kuomba maghfirah kwa Mola Mtukufu, kisha jiepushe na maasi yote kwani maasi yanamzuia mja kushika maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema:
" إن الرجل ليحرم العلم بالذنب يصيبه "،
"Hakika mtu hunyimwa elimu kwa dhambi anazozitenda"
Imaam Ash-Shaafi'iy (Rahimahu-Llaah) alikuwa mwepesi wa kuhifadhi Qur-aan lakini Qur-aan ilipokuwa nzito kuihifadhi alisema:
"شكوت الى وكيع سوء حفظي فأرشدني إلى ترك المعاصي و أخبرني بأن النور علم و نور الله لا يؤتاه عاصي"
"Nililalamika kwa Wakiy’i kuhusu kushindwa kuhifadhi Qur-aan akaninasihi kuacha maasi na akanijulisha kuwa mwanga ni elimu na mwanga wa Allaah haumfikii mwenye kuasi"
Kutoshughulika na anasa za dunia
Inampasa mwenye kutaka kuhifadhi Qur-aan auhifadhi wakati wake mwingi kwa ajili ya kuhifahdi Qur-aan. Ajitenge na anasa za dunia asizichanganye na kazi hii, ili akili yake, na moyo wake upate utulivu kwa ajili ya hifdhwul-Qur-aan. Ni muda mwingi leo hii watu hupoteza masaa mengi kutazama televisheni na kukaa mabarazani au kwenye nyumba zilizotawaliwa na mazungumzo ya kidunia yasiyokwisha.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((مَا جَعَلَ اللَّهُ لِرَجُلٍ مِّن قَلْبَيْنِ فِي جَوْفِهِ))
((Allaah Hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake)) [Al-Ahzaab: 4]
Kipaumbele kwa wakati maalumu kila siku
Ni lazima ujiwekee wakati maalumu kila siku iwe ni kipaumbele katika ratiba zako za kila siku kwa ajili ya kuhifadhi Qur-aan. Na wakati bora kabisa ulioonekana kuwa ni muwafaqa kwa hifdhw ni nyakati za ukimya ambazo hakuna vishawishi vya kukukatiza hifdhw yako, kama simu, watu ingia toka, sauti nyinginezo zozote, na nyakati nzuri ni zile za usiku, karibu na alfajiri, au alfajiri kabla ya kujaza lolote jengine katika bongo lako.
Tuesday, October 30, 2012
NJIA ZA KUKUWEZESHA KUHIFADHI QURAN. (01)
01 Fadhila Za Kuhifadhi Qur-aan.
Hifdhwul-Qur-aan (kuhifadhi Qur-aan) hakika ni jambo muhimu la kuazimiwa na Muislamu kwani fadhila zake ni nyingi na tukufu mno.
Makala katika kiungo kifuatacho inaelezea fadhila hizo kwa kirefu:
02 Qur-aan Ni Uongofu Kamili
Qur-aan ni Kitabu Alichotuteremshia Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kutoka mbinguni, nacho kwetu ni; nuru (mwanga) unaotunawirisha, kamba nene, nzito isiyokatika, mizani ya uadilifu, poza ya moyo, uongofu kamili, na sababu ya furaha na kufaulu kwa binaadamu katika dunia yake na akhera yake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلاَوَتِهِ أُوْلَئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ)
((Wale tuliowapa Kitabu, wakakisoma kama ipasavyo kusomwa, hao ndio kweli wanakiamini)) [Al-Baqarah: 121]
03 Umri Bora Wa Kuhifadhi Qur-aan
Umri mzuri utakaorahisisha kuhifadhi Qur-aan ni baina ya umri wa miaka mitano hadi ishirini na tatu taqriban, kwani binaadamu katika umri huu huweza kuhifadhi kwa wepesi kabisa na bongo huwa na kumbukumbu nzuri bado na sio wepesi kusahau unachokihifadhi. Amesadikisha maneno yake ambaye amesema:
"الحفظ في الصغر كالنقش في الحجر، والحفظ في الكبر كالنقش على الماء "
"Kuhifadhi udogoni ni kama nakshi katika jiwe, na kuhifadhi ukubwani ni kama nakshi katika maji.
Maana yake ni kuchora au kuandika katika udongo uliomaji bado, maandishi au mchoro huo hubakia milele kuwa ni alama katika jiwe litakapokauka. Ama mwenye kuchora katika maji, hutoweka.
Hivyo ni fursa tukufu Muislamu kuitumia katika umri huu kuhifadhi maneno ya Mola wake, na kama fursa hii imekupita basi wahifadhishe watoto wako wa kiume na wa kike usiache fursa hii ikawapita na wao pia kwani furaha ya wao kuhifadhi Qur-aan itakuwa ni furaha na fakhari kwako pamoja na ridhaa ya nafsi yako. Vile vile mzazi mwenye kumhifadhisha mwanawe Qur-aan atakuwa ameshatanguliza huko Akhera akiba na fadhila zake na za mwanawe.
Hata hivyo, endapo utakupita umri huo kusiwe ni sababu ya kukufanya usiweze kuhifadhi Qur-aan, kwani hii ni sababu wengi wanaitumia kwamba akili ni dhaifu ya kuhifadhi au umri ushakuwa mkubwa akili haikamati n.k. Hakika hakuna sababu yoyote ya kumzuia mtu asiweze kuhifadhi Qur-aan, kwani haya ni maneno ya Mola wetu Mtukufu Aliyetuumba na Ambaye Ametuahidi kwamba ni maneno mepesi kuhifadhi kwa yule mwenye dhamira khaswa. Allaah Amerudia ahadi Yake mara nne katika Surah moja:
((وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ))
((Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur-aan iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anayekumbuka?)) [Al-Qamar: Aayah Namba 17, 22, 32 na 40]
Kwa hiyo inampasa mtu awe na imani, yakini na maneno ya Mola Wetu, kuwa na dhana njema, kuwa na matumaini na matarajio mazuri daima, na hivi ndivyo itakavyokupa nguvu zaidi ya kuhifadhi hadi ufikie upeo wake.
SOMO LITAENDELEA........
Subscribe to:
Posts (Atom)

